Wednesday, August 7, 2013

Aliye mpiga Dr Ulimboka afutiwa kesi

MKURUGENZI wa Mashitaka nchini (DPP), Dk.
Eliezer Feleshi, amefuta kesi ya kuteka na kujaribu
kumuua Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari
nchini, Dk. Steven Ulimboka, iliyokuwa ikimkabili
raia wa Kenya, Joshua Mulundi, katika Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
Hatua hiyo imeelezwa kuwa ni baada ya DPP
kuona hana haja ya kuendelea kumshitaki kwa
makosa hayo ambayo yalikuwa hayana dhamana.
Hati hiyo ya DPP iliwasilishwa chini ya kifungu
cha 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya
Jinai ya mwaka 2002 kwa niaba yake na Wakili
Mwandamizi wa Serikali, Tumaini Kweka, jana
mbele ya Hakimu Mkazi Waliarwande Lema.
Kweka aliiambia mahakama kuwa kesi hiyo ilikuja
kwa ajili ya kutajwa lakini upande wa Jamhuri
hauna nia tena ya kuendelea kumshitaki Mulundi
kwa kesi hiyo.
Hakimu Lema alikubaliana na hoja hiyo na
akamfutia kesi hiyo Mulundi ambaye yupo
gerezani tangu Julai 13, mwaka jana.
Hata hivyo muda mfupi baada ya Hakimu Lema
kumfutia kesi hiyo Mulundi, askari kanzu
walimkamata tena na kumfikisha kwa Hakimu
Mkazi, Alocye Katemana na kisha Wakili Kweka
akaiambia mahakama kuwa upande wa Jamhuri
umemfungulia kesi mpya ambayo itakuwa na
shitaka moja tu.
Mbele ya Hakimu Katema, wakili huyo alidai kuwa
Julai 3, mwaka jana, Mulundi katika Kituo cha
Polisi Oystebay alitoa taarifa za uongo kwa ofisa
wa polisi kuwa yeye na wenzake walikodiwa
kwenda kumteka na kumjeruhi Dk. Ulimboka,
jambo ambalo si kweli.
Alidai kosa hilo ni kinyume cha kifungu cha 122
cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002
na kuongeza kuwa upelelezi wa kesi hiyo mpya
umekamilika.
Wakili Kweka alidai licha ya kosa hilo kuwa na
dhamana kwa mujibu wa sheria, lakini upande wa
Jamhuri unaomba Mulundi asipewe dhamana kwa
ajili ya usalama wake.
Hakimu Katemana aliiahirisha kesi hiyo kwa
muda na kisha kuutaka upande wa Jamhuri uende
ukalete kwa maandishi hati ya kumfungia
dhamana mshitakiwa huyo.
Hata hivyo mshitakiwa huyo alikanusha shitaka
hilo na akaomba apewe dhamana kwani alikuwa
na wadhamini. Pia alidai amesota muda mrefu
gerezani bila kosa.
“Ninajua wanataka kunifungia dhamana makusudi
ili waweze kunyamazisha Bunge na umma
usiendelee kupiga kelele kuhusu tukio la kupigwa
na kuteswa kwa Dk. Ulimboka na kwa taarifa yenu
mkinipeleka tena gerezani naenda kuanza mgomo
…nimechoka kuonewa,” alidai Mulundi.
Hata hivyo kesi hiyo iliporudi tena mchana,
Wakili Kweka hakuweza kuja na hati ya kuzuia
dhamana, hali iliyosababisha Hakimu Katemana
kutoa masharti ya dhamana kwa mshitakiwa
huyo.
Hata hivyo mshitakiwa huyo jana alishindwa
kutimiza masharti hayo na Hakimu Katemana
aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 20, mwaka huu.
Katika kesi hiyo awali, Wakili wa Serikali, Ladslaus
Komanya, mbele ya Hakimu Agnes Mchome,
alidai kuwa Mulundi Juni 26, mwaka jana, akiwa
eneo la Leaders Club alimteka Dk. Ulimboka.
Katika shtaka la pili, Komanya alidai kuwa Juni
26, mwaka huu, akiwa katika eneo la Msitu wa
Mabwepande, Tegeta, Dar es Salaam, kinyume cha
sheria, mshtakiwa huyo alijaribu kumsababishia
kifo Dk. Ulimboka.

No comments:

Post a Comment